Tuwache lalama na tuunge Harambee Stars Afcon inapoanza – Taifa Leo

Na CECIL ODONGO

MWISHONI mwa wiki hii, mashindano ya Taifa Bingwa Afrika (AFCON) yanatarajiwa kung’oa nanga huku Kenya kwa mara ya pili kwenye historia ikishiriki.

Vijana wa kocha Sebastien Migne wanatarajiwa kuwasili nchini Misri kesho baada ya kushiriki mazoezi Ufaransa kwa muda wa majuma mawili.

Stars vile vile ilishiriki mechi za kirafiki dhidi ya Madagascar na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Huku Stars ikitarajiwa kupepetana na Algeria kwenye mechi yao ya kwanza Jumapili saa tano usiku, ni wakati wa mashabiki na Wakenya kwa jumla kuunga mkono vijana wetu wanapojizatiti kurejesha hadhi ya zamani ya Kenya kama miamba wa soka Afrika Mashariki na Kati.

Ni wazi kwamba mashabiki wengi hawakuridhishwa na jinsi kikosi cha taifa kilivyoteuliwa.

Hata hivyo, hili halifai kuzua mgawanyiko zaidi kwa sababu Kenya ni taifa moja na liwalo liwe, sisi sote tunafaa kuungana kutakia timu yetu matokeo mazuri.

Nasema hivyo kwa sababu tangu kikosi cha mwisho kitajwe na kocha Migne wiki jana, mashabiki wamezamia katika mitandao ya kijamii kutoa lalama zao.

Shutuma zaidi zilichipuka baada ya mechi ya kirafiki dhidi ya DRC, ambapo wengi wa mashabiki walimponda Migne hasa kutokana na makosa aliyofanya mnyakaji wa Starsl, Patrick Matasi.

Cha kusikitisha ni kwamba baadhi ya mashabiki hata hawakuwa na haya kutangaza kuwa wataishabikia timu ya taifa ya Tanzania na kuasi Harambee Stars huku wakiomba ipigwe kwenye mechi zote.

Jameni, uzalendo wetu upo wapi ikiwa makosa madogo madogo kama wachezaji kutojumuishwa kikosini kinatufanya tukimbilie kuunga taifa jirani, ambalo nina imani mashabiki hao hawajui hata mchezaji wao mmoja?

Tunafaa kama Wakenya kuwa wazalendo katika kila hali. Jambo hili litasaidia kuonyesha upendo wetu kwa nchi na pia kuwatia moyo wachezaji wetu kwani watakuwa wakifahamu taifa zima liko nyuma yao, na lina matarajio makubwa kutoka kwao.

Wachezaji watakaopangwa kikosini nao wanafaa kutumia fursa hii ambayo ni ngumu kucheza kwa kujituma na kudhibitishia wakosoaji kwamba wanaweza kutambisha taifa kwenye kipute hicho.

Kwa wanasoka ambao walitemwa ama kutoorodheshwa, huu ni muda mwafaka wa kutazama kipute cha AFCON na kujifunza mengi kwa minajili ya kuendeleza vipaji vyao.

Kila la kheri Harambee Stars na tuna wingu la matumaini mtawakilisha taifa vizuri.


Posted

in

by

Tags: