Rekodi muhimu kuhusu Sharon na Melon zakosekana hospitalini.

Magazeti ya Kenya Jumanne, Juni 18 yanaripoti kuhusu wafuasi wa Naibu Rais Wiliam Ruto kutoa hisia zao dhidi ya matamshi ya Rais Uhuru Kenyatta.

Pia magazeti haya yanaangazia mikakati iliyowekwa na serikali ya Kenya katika mipaka yake ili kuzuia ugonjwa wa Ebola kuingia nchini.

The Standard

Katika gazeti hili, tunaarifiwa kuwa pacha wa Kakamega hawatafanya mitihani yao ya kitaifa (KCSE) mwaka huu ilivyokuwa ikitarajiwa.

Licha ya ukweli kufichuka kuhusu wazazi na uhusiano wa Sharon Mathias, Melonya Lutenyo na Mavis Imbaya, watatu hao watarejea katika kidao cha tatu.

Kulingana na gazeti hili, wasichana hao walipoteza muda mwingi wakiwa nje ya shule kutafuta mizizi yao pia matokeo ya DNA yanaweza kuathiri mawazo na fikra zao masomoni.

Wakati wa mkutano wa familia husika mnamo Jumatatu, Juni 18, familia zote ziliafikiana kuwa warembo hao wataendelea kuishi katika makazi waliyolelewa bila ya ubaguzi.

Hata hivyo, kila mmoja ana uhuru ya kumtembelea mamake mzazi wakati wowote.

Familia hizo pia ziliafikiana kutoishtaki Hospitali ya rRufaa ya Kaunti ya Kakamega walikozaliwa watatu hao.

People Daily

Katika gazeti hili, hakuna mwinjilisti yeyote atakayeruhusiwa kufunganisha ndoa bila cheti cha maadili kutoka kwa idara ya jinai (DCI).

Sheria hii itaanza kutekelezwa iwapo mapendekezo ya Mwanasheria Mkuu Paul Kihara yatapitishwa.

Mapendekezo hayo yanapania kukabiliana na idadi kubwa ya visa vya kupeana talaka ambavyo vinaendelea kushuhudiwa nchini, kwa hivyo sheria hiyo kuwa njia moja ya kukuza ndoa.

Pia wachungaji watalazimika kuweka wazi cheti cha kuonyesha kusajiliwa kwa kanisa husika, cheti cha kuwa mwanachama wa kanisa hilo na barua ya kumpendekeza kutoka kanisani.

Wanandoa watakaotaka kutalikiana, watahitajika kuwa wamekaa katika ndoa hiyo kwa muda wa miaka mitatu na pia kwa kutoa thibisho kuwa njia zote za kusuluhisha tofauti zao ziligonga mwamba.

The Star

Gazeti la The Star, linaripoti kuwa viongozi ambao ni wafuasi wa naibu rais, wamemkashifu rais kwa kuonekana kuwa katika njia panda.

Mwakilishi wa wanawakeKkaunti ya Kirinyaga, Wangui Ngirici, anadai kuwa Uhuru alikuwa tayari kuwakemea viongozi katika kundi la Tanga Tanga kwa sababu za kampeni za mapema huku akionekana kutowasuta wanachama wa kundi la Kieleweke ambao pia wanaendesha kmpeni zao dhidi ya Ruto.

Mbunge wa Mukuruweini Anthony Kiai anadai kuwa matamshi ya Uhuru yalikuwa ya kukera na yalizidisha mgawanyiko katika Chama cha Jubilee.

Kiai pia anadokeza kuwa ingekuwa vyema kwa rais kuwaita katika mkutano wa pembeni badala ya kuwaibisha hadharani.

Daily Nation

Katika gazeti hili Wizara ya Afya imekanusha madai kuwa ugonjwa wa Ebola umeingia nchini.

Wizara hiyo imethibitisha kuwa matokeo kuhusu chembechembe za damu ya mwanamke aliyekuwa akidaiwa kuwa na dalili za ugonjwa huo, yanaonyesha kuwa hakuwa ameathirika kwa hivyo kutangaza kuwa nchi hii ni salama dhidi ya Ebola.

Takriban maafisa 169 wa afya wametumwa katika mipaka yote ya Kenya ili kupima kila mtu anayeingia nchini.

Maafisa 30 wamekita kambi katika uwanja wa ndege wa JKIA, huku maeneo ya Nyanza, Magharibi na Bonde la Ufa yakiwa chini ya ulinzi mkali kwa sababu ya kuwa karibu na Uganda.

3. Taifa Leo

Katika gazeti hili, shughuli ya kutafuta stakabadhi muhimu za hospitalini kuhusu Sharon na Melon zimekosa kufua dafu.

Kulinagana na gazeti hili, maafisa katika Hospitali ya Rufaa ya Kakamega wanasema kuwa taarifa kuhusu pacha hao waliozaliwa hospitalini humo lakini wakatenganishwa miaka 19 iliyopita kisha kupewa mama tofauti hazipatikani.

Waziri wa afya wa kaunti hiyo Rachael Okumu, alisema rekodi zingine ambazo zingeonyesha kilichotendekeka baada ya pacha hao kuzaliwa huenda ziliharibiwa baada ya muda uliowekwa kisheria kukamilika, na hivyo ni vigumu kujua kilichotokea.

Okumu alisema kuwa hospitali hiyo haina chochote cha kuficha kuwahusu pacha hao, na hivyo wakaamua kupokeza wapelelezi nyaraka zilizopatikana kwa uchunguzi zaidi.

Source: Tuko.co.ke


Posted

in

by

Tags: